Featured

Taarifa ya Mamlaka ya Dawa na Chakula TFDA Kuhusu Dawa Bandia Zilizokamatwa

Na Ally Daud

MADAWA bandia na yasiyo sahihi kwa matumizi ya binadamu yamekamatwa maeneo ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya kufanyika ukaguzi maalum wa kutafuta dawa bandia katika maeneo hayo iliyofanyika hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati wa kutoa Matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa uliofanyika katika mikoa ya Kanda za Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.

“Kutokana na ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda za Ziwa pamoja na Nyanda za Juu Kusini wa kutafuta dawa bandia na zisizo sahihi kwa matumizi ya binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia za aina tano ambazo zipo kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua vijasumu(Antibiotics)” alisema Bw. Sillo.

Aidha Bw. Sillo amesema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata dawa ya malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa katika kiwanda cha Elys Chemical  nchini Kenya na nyingine zinatengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.

Mbali na hayo Bw. Sillo amesema kuwa pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi hilo lilifanikiwa kubaini na kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi , zisizosajiliwa na zenye ubora duni zenye thamani ya Tsh. Milioni 17.463.

Bw. Sillo ameongeza kuwa Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali ambazo zilionyesha uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara mwezi Agosti na Septemba mwaka huu  na kusistiza kwamba zoezi hilo la ukaguzi linaendelea nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa hatua stahiki.

Kwa upande wa Msajili wa  Baraza la famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema kuwa wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi.

“Wataalamu wa dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.

Zoezi hilo la Ukaguzi maalum wa dawa bandia ulianza Oktoba 4 mwaka huu linafanywa kwa ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi pamoja na Maafisa kutoka Baraza la Famasi litakuwa endelevu ili kuhakikisha dawa bandia zinatoweka nchini.

Waziri Mkuu: Tumieni Misikiti Kuhubiri Misingi ya Uislamu



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Waislamu watumie nyumba za ibada kuhubiri uislamu na misingi yake.

Ametoa wito huo jana mchana (Ijumaa, Oktoba 28, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Nunge mjini Dodoma.

Alisema dini ya Kiislam inafundisha kwamba sala ndiyo msingi mkubwa unaopaswa kufuatwa na kila muumini hivyo ni lazima wafanye ibada kwa wakati.

“Nasisitiza kwamba wote tutumie muda wetu vizuri pamoja na mambo mengine tufanye ibada kwani dini inatuekeza kuwa sala ndiyo msingi mkubwa kwenye Uislamu. Tunayo kazi ya kuimarisha misingi ya dini kwa kutumia nyumba za ibada,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Waislamu wana jukumu la kufundisha watoto wao na kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.

“Dini inajenga maadili mema kwa mtoto na hata mtu mzima. Pia dini inajenga misingi ya uvumilivu na inamuwezesha mtu kumtambua Mwenyezi Mungu. “Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa waumini wenzake wa mkoa wa Dodoma baada kuhamia rasmi, ameahidi kutoa ushirikiano kwao na pia amewaomba wampe ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Nimekuja kujitambulisha. Mimi ni kijana wenu, ndugu yenu. Nimekuja Dodoma rasmi nyumbani na kikazi. Naomba mnipokee na naamini katika kipindi chote nitakachokuwa hapa nitapata ushirikiano nanyi na pia nitawapa ushirikiano,” alisema.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwaomba waumini hao wawaombee dua wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanatarajia kuanza mitihani ya kuhitimu Novemba Mosi, mwaka huu ili waweze kufaulu.

Waziri Mkuu aliwaomba waumini hao waendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.

Aidha, Waziri Mkuu alichangia sh. milioni moja kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa zahanati katika msikiti huo. Miradi inayojengwa na waumini wa msikiti huo kwa sasa ni zahanati, madarasa ya shule ya awali na shule ya ufundi.

Benk ya Twiga Bancorp Yafilisika....BoT Yachukua Usimamizi Wake Kunusuru Amana za Wateja wa Benki Hiyo



Benki Kuu ya Tanzania imetangaza rasmi kuchukua usimamizi wa Benki ya Twiga Bancorp kuanzia jana kutokana na upungufu wa mtaji wa benki hiyo kiasi cha kuwa na deni la Shilingi Bilioni 21.

Benki Kuu pia imesimamisha shughuli zote za utoaji huduma za kibenki za benki hiyo kwa kipindi kinachokadiriwa kufikia wiki moja kuanzia jana tarehe 28/10/2016 ili kutoa nafasi kwa ajili ya kupanga taratibu za uendeshaji wa benki hiyo.

Maamuzi hayo yametangazwa jana jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndullu mbele ya waandishi wa habari, na kusema kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 56 (1)(g)(i) na 56(2) a-d cha taasisi za fedha ya mwaka 2006.

"Uamuzi huu umechukuliwa baada ya kubaini kuwa benki ya Twiga ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga kutaharisha usalama wa amana za wateja" Imesema sehemu ya taarifa ya Prof. Benno Ndullu.

Aidha, amewataka watu wote wanaodaiwa na benki hiyo kulipa madeni yao kupitia Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba wadaiwa wote watafuatiliwa kokote waliko.

Mbali na maamuzi hayo, benki hiyo pia imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa benki hiyo, huku ikimteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za benki hiyo kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa benki hiyo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa usimamizi wa mabenki Bw. Keddedy Nyoni amesema benki hiyo ilianza na mtaji wa bilioni 7.5 lakini sasa ina deni la hadi bilioni 21.

Jaji Lubuva Ataka Tume ya Uchaguzi Ifumuliwe.......



Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.

Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).

Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati akikabidhi taarifa ya tathimini baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.

Lubuva alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana.

“Pamoja na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa uhuru zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema.

Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.

“Tathimini hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha mzunguko wa uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,” alisema.

Alisema changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha.

Pia wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.

Alisema tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

“Baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupiga kura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura wengi, pia wapigakura walijiandikisha katika daftari la kudumu kwa ajili ya matumizi mengine ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo wa hofu, vitisho na vurugu siku ya kupigakura,” alisema.

Waziri Mhagama, Mkurugenzi wanena
Kwa upande wake, Waziri Mhagama alisema tume inapaswa kupongezwa kwa kukamilisha zoezi zima la Uchaguzi Mkuu, ambalo lilikuwa na changamoto nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa.

Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura 343, tume inapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine, lakini haikuwezekana kufanyika hivyo baina ya mwaka 2010 na mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema sababu hizo ni pamoja na ufinyu wa bajeti na kuchelewa kupatikana kwa fedha kwa wakati, lakini serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa mapungufu yaliyo ndani ya uwezo wake, yanatatuliwa ili kuiwezesha tume kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria kwa wakati.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ilifanyika, ikiwa ni hatua ya kukamilisha mzunguko wa uchaguzi.

Alisema kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa, watendaji 929 ambao ni sawa na asilimia 90.3 walisema wana uelewa kuhusu muundo wa tume na watendaji 100 sawa na asilimia 9.7, walikuwa hawana uelewa kuhusu muundo wa tume.

“Kati ya watendaji 929 wa uchaguzi waliohojiwa, 818 sawa na asilimia 88 walisema kuwa muundo wa tume unafaa kuendesha uchaguzi, aidha watendaji 111 sawa na asilimia 12 walieleza kuwa muundo wa tume haufai katika kuendesha uchaguzi,” alisema.

Pia matokeo yanaonesha kuwa, katika watendaji wa uchaguzi 1,014 waliohojiwa, 814 sawa na asilimia 80.3 walisema hakukuwa na changamoto katika njia hizo, watendaji 200 sawa na asilimia 19.7 walieleza njia za mawasiliano zilikuwa na changamoto.

Alisema matokeo ya tathimini yameonesha kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa 996 sawa na asilimia 96.8 walikuwa na maoni kuwa utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi ulizingatia maelekezo yaliyotolewa na tume, ambapo watendaji 33 sawa na asilimia 3.2 walieleza kuwa utekelezaji haukuzingatia maelekezo hayo.

Aidha alisema wadau wa uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu uelewa wao juu ya elimu ya mpiga kura, kati ya wadau 1,463 sawa na asilimia 76.4 walisema walikuwa na uelewa wa elimu ya mpiga kura na 452 sawa na asilimia 23.6 hawakuwa na uelewa.

Kailima alisema wapiga kura 499 walihojiwa, ambapo kati yao wapiga kura 377 sawa na asilimia 75.6 walisema walitumia chini ya dakika 30 kufika kituo cha kupiga kura, wakati wapiga kura 87 sawa na asilimia 17.5 walitumia dakika 30 hadi 60 kufika kituo cha kupiga kura.

CCM Yatekeleza Agizo la Rais Magufuli kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications



Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetekeleza agizo la Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho la kuwalipa mishahara na haki zao nyingine zinazofikia Sh milioni 609 wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications (UPL) wanaozalisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo mwezi uliopita alipofanya ziara ya ghafla katika ofisi ya magazeti hayo na kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi na baadaye kuagiza ndani ya mwezi huo, wafanyakazi walipwe mishahara na haki zao zote.

Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema pia miongoni mwa maagizo ya Rais Magufuli ni kutaka wafanyakazi hao kutobughudhiwa wala kufukuzwa kazi baada ya kueleza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha wanalipwa haki zao.

“Nataka kuwahakikishia mpaka hapa tunapozungumza sasa hivi hatudaiwi tumeishatekeleza maagizo ya Mwenyekiti, tuko safi labda katika sehemu nyingine,” alisema.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliagiza kupatiwa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na pia aliagiza kulipwa kwa deni linalodaiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF kutokana na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi.

Katika mazungumzo yao na Rais, wafanyakazi walilalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutowasilishwa kwa michango ya wafanyakazi kwa NSSF, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti katika hali ya kutatanisha, kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya wafanyakazi, kutolipwa kwa madeni wanayozidai taasisi za serikali na wanaostaafu kutolipwa mafao yao.

Mmiliki wa Shule Iliyofutiwa Matokeo Ya Darasa la 7 Amwaga Machozi Hadharani



Siku moja baada ya matokeo ya darasa la saba kutangazwa, baadhi ya wamiliki wa shule wamelijia juu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kufuta matokeo ya wanafunzi wao, huku mmoja wao akibubujikwa na machozi akidai wamehujumiwa.

Ikitangaza matokeo hayo juzi, Necta ilisema imefuta matokeo ya wanafunzi 238 kwa sababu ya udanganyifu, ikiwatuhumu wakuu wa shule sita na walimu kuhusika kuiba mitihani, kuwapa majibu watahiniwa au kuwafanyia mtihani.

Necta ilienda mbali zaidi na kudai kuwa kwenye shule moja, walimu walijificha bwenini, chooni na ofisini ambako wanafunzi waliwafuata na kupewa majibu na baadaye kuyasambaza kwa wenzao.

Lakini, walimu hao  wamepinga vikali tuhuma hizo za kushiriki katika udanganyifu, isipokuwa shule moja tu ambayo ilisema mwalimu aliyehusika ameshachukuliwa hatua.

“Sijafurahishwa na kitendo cha Necta kuifutia matokeo shule yetu. Hiyo ni hujumu,” alisema mmiliki wa shule ya msingi Tumaini iliyopo Sengerema mkoani Mwanza, Kandumula Maunde.

Huku akilia, Maunde alisema wakati tukio hilo lilotokea saa 5:00 asubuhi, hakuwepo na hakushirikishwa.

“Niliitwa kesho yake na kupata maelezo kuwa wanafunzi wa shule yako wamekamatwa kwa sababu wameandikiwa majibu ya mtihani kwenye sketi, sikukubaliana nao,” alisema.

Kwa mujibu wa Necta, mmiliki huyo aliiba na kuandaa majibu ambayo watahiniwa wake waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani.

Necta imewataja waliohusika kuwa ni mmiliki aliyetajwa kwa jina la Jafari Maunde, msimamizi anayeitwa Alex Kasiano Singoye na wanafunzi wote.

Alisema hakukubaliana na kitendo hicho kwa sababu wanafunzi hao walikuwa wameandaliwa vizuri kujibu mitihani yao.

Maunde aliliomba baraza la mitihani kupitia upya uamuzi wake wa kuifutia shule hiyo matokeo kwa kuwa umeathiri maisha ya wanafunzi waliokuwa na ndoto za kuendelea na masomo.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliofutiwa matokeo waliiomba Necta kuangalia upya uamuzi huo. Wanafunzi hao walieleza kuwa msimamizi wa mtihani wa siku hiyo alikuwa akiwasumbua na aliwalazimisha waandike maelezo ya kukiri kuwa walikamatwa na majibu.

“Msimamizi alitulazimisha tuandike kwenye ubao baada ya kumaliza mitihani maelezo yakisema tumekamatwa na majibu ya mtihani yakiwa yameandikwa kwenye sketi tulizokuwa tumevaa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao, Kefa Matini.

Kwa upande wa shule ya msingi ya Little Flower iliyopo Serengeti mkoani Mara, walimu walisema uamuzi wa kufutiwa matokeo ni adhabu isiyostahili.

Wanafunzi 37 wa shule hiyo  inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Parokia ya Magumu wamefutiwa matokeo.

Necta imeeleza kuwa mwalimu mkuu wa Little Flowers aliiba mtihani, kuandaa majibu na kumpa msimamizi mkuu pamoja na wasimamizi wengine ili wawape watahiniwa.

Imesema waliohusika ni mwalimu mkuu anayeitwa Cecilia Nyamoronga, msimamizi mkuu (mwalimu), Haruni Mumwi na msimamizi (mwalimu), Genipha Simon na watahiniwa wote.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Paskael Chacha alisema uamuzi huo umewaumiza walimu na watoto waliofanya mtihani walioko shuleni na wazazi kwa kuwa hawajapewa sababu za udanganyifu huo na ulimhusisha nani na lini.

“Walimu hawakuwepo shuleni, mkuu wa shule ndiye alikuwa akiruhusiwa kuwepo shuleni kwa muda mfupi. Inanipa shida kujua udanganyifu ulifanyikaje na ulimhusisha nani.

"Hili suala linatupa shida kwa kuwa wasimamizi walioletwa siku ya kwanza si waliofika kusimamia. Sasa taarifa kama hizi zinauma sana,” alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa taarifa zinazodai kuwa siku ya mtihani mtoto mmoja alikamatwa na karatasi ya majibu na kumtaja mkuu wa shule kuwa ndiye aliyempa, mwalimu huyo alikana na kudai kuwa hana taarifa.

Majibu ya Dr. Msonde
Akizungumzia malalamiko hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema wanaosema wameonewa wanatakiwa kuomba radhi na kukubali adhabu kwa sababu waliokamatwa walikutwa na uthibitisho, akitoa mfano wa Shule ya Msingi Tumaini.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Little Flower, Dk Msonde alisema ofisa wa baraza la mitihani alishuhudia mwalimu akipitisha karatasi ya majibu kwa wanafunzi .

“Sasa hapo utasema umeonewa? “Tumezoea kuona (matukio ya udanganyifu) yale ya mwanafunzi mmoja, lakini haya yanatisha. Mwalimu au msimamizi anamsaidia mwanafunzi, hii si sawa,” alisema.
Older Posts
© Copyright BONGO-PERFECT Published.. Blogger Templates
Back To Top