Featured

CCM Yatekeleza Agizo la Rais Magufuli kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications



Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetekeleza agizo la Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho la kuwalipa mishahara na haki zao nyingine zinazofikia Sh milioni 609 wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications (UPL) wanaozalisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo mwezi uliopita alipofanya ziara ya ghafla katika ofisi ya magazeti hayo na kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi na baadaye kuagiza ndani ya mwezi huo, wafanyakazi walipwe mishahara na haki zao zote.

Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema pia miongoni mwa maagizo ya Rais Magufuli ni kutaka wafanyakazi hao kutobughudhiwa wala kufukuzwa kazi baada ya kueleza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha wanalipwa haki zao.

“Nataka kuwahakikishia mpaka hapa tunapozungumza sasa hivi hatudaiwi tumeishatekeleza maagizo ya Mwenyekiti, tuko safi labda katika sehemu nyingine,” alisema.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliagiza kupatiwa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na pia aliagiza kulipwa kwa deni linalodaiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF kutokana na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi.

Katika mazungumzo yao na Rais, wafanyakazi walilalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutowasilishwa kwa michango ya wafanyakazi kwa NSSF, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti katika hali ya kutatanisha, kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya wafanyakazi, kutolipwa kwa madeni wanayozidai taasisi za serikali na wanaostaafu kutolipwa mafao yao.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright BONGO-PERFECT Published.. Blogger Templates
Back To Top